Lourdes- Ufaransa |
Miaka kadhaa imepita
tangu nilipofanya hija kwenda sehemu ya
kuhiji kati ya maeneo makubwa zaidi duniani ambayo mama Bikira Maria alitokea
mara kadhaa na kufanya miujiza mingi ikiwemo kuponya wagonjwa. Mji huu unaitwa
Lourdes ni mji ulipo katika nchi ya Ufaransa ambapo mama Bikira Maria alimtokea
msichana maskini Bernadeta Subirou. Tunaambiwa
kwamba, kati ya records za uponyanyaji zilizopo, Lourdes (Lurdi) inaongoza kwa
idadi ya uponyaji. Ingawa Mt. Bernadetha hakuahidiwa maisha marahisi hapa
duniani, basi sasa anafurahi mbinguni kama Mtakatifu lakini pia, mwili wake
haujaoza toka alipokufa mwaka 1879 hadi leo hii.
Mt. Bernadeta Soubirous |
Siku kadhaa zilizopita,
Fr. Richard Matanda (Napenda kumuita mtume
wa mama Bikira Maria kwani naona jinsi anavyompenda na anavyoeneza ibada
ya mama huyu mwema kwakwe ndio maana nimependa kumuita hivyo) aliniomba niweze
kuwashirikisha watu hasa wale wanaofuatilia makala zake kumuhusu mama, juu ya
safari yangu ya hija huko Lurdi Ufaransa.
Safari hiyo niliifanya
mwaka 2009 wakati huo nilikuwa nikiishi katika nchi ya Uswiss na nchi hii ilipakana
sana na nchi ya Ufaransa ingawa safari ya kwenda Lurdi kwa treni ni safari ya
siku nzima. Hata hivyo, sikuchukua hatua yoyote ya kutembelea eneo lile.
Pengine nilidhani hija ni kwaajili ya watu fulani na sio mimi, pengine ni
kwaajili ya watu wenye magonjwa na udhaifu fulani wa kimwili na sio mimi.
Kwakweli sababu kubwa ya kutokwenda sikuijua. Kuna siku niliwaza sana
nikamwambia mama Maria kwamba nikirudi likizo nitakuja kukutembelea. Mwezi July
mwaka huo huo 2009 nilirudi Tanzania kwa likizo kwa muda wa mwezi mmoja na
niliporudi kazini kwangu huko Uswisi safari hii nilifikiria sana kuhusu Lurdi
lakini sikupata jibu. Kila mara mimi na rafiki zangu tulipanga kutembelea mji
huu au ule lakini sikuwahi kusema Lurdi.
Siku moja, nikakumbuka
ile ahadi yangu ya kwenda hija lakini sikutaka kwenda na ukikumbuka kwamba
marafiki zangu wengi walikuwa aidha wapagani au Wakristu wasioamini tena,
ilikuwa ngumu kupata rafiki wa kwenda
nae. Basi baana ya kuona wazo lile linaninagi sana, nikamwambia mama "
Ukinipa malaika wa kwenda naye, nitakwenda." Siku hiyo jioni nilikutana na
rafiki yangu mmoja niiyeishi naye sehemu
moja. Rafiki yangu aliitwa Gisselle (Gisela kwa Kiswahili) yeye alitoka
nchi ya Benin na alikuwa akiongea Kifaransa vizuri sana. Sikumbuki tuliongea
nini ila nikasema natamani kwenda Lurdi, akasema hata mimi twende wikendi hii.
Vincenzia- Marie na Gissele wakiwa Lurdi |
Basi hivyo ndivyo mama
alivyonipa malaika wa kwenda naye huko Lurdi. Tulitafuta hoteli tukafanya
booking na vilevile tulinunua tiketi za treni tayari kwa safari. Tuliondoka
Ijumaa usiku wa saa 4 na tuliwasili
Lurdi saa 12 kamili asubuhi. Tulienda
hotelini kuoga kisha tukateremka kwenda
eneo la tukio. Lurdi ina maeneo kadhaa ya kutembelea lakini maeneo makubwa sana
na yanayojaa watu ni yale ya Pangoni mahala aliposimama kabisa mama Bikira
Maria na kwenye visima vya kuoga katika
maji ambayo yalitokea baada ya mama Bikira Maria kumwambia atafune majani
machungu na kuyatema kisha ikatokea chemchem ya maji, kisha, mama B. Maria
akasema watu wanywe yale maji na wanawe
uso watapona. Basi serikali ya ufaransa ikajenga visima vya kuoga na sehemu ya kuchota maji. Pia kuna makanisa,
njia ya msalaba n.k . Lakini sehemu hizi za pango na Visimani foleni yake huwa
ndefu sana na watu hujihimu asubuhi mno. Hatukuwa na muongoza msafara so
tukajifanyia safari wenyewe kuanzia kanisani, njia ya msalaba na kanisani tena.
Kuna makanisa makubwa kama matatu hivi.
Njia ya Msalaba |
Njia ya Msalaba |
Njia ya Msalaba |
Njia ya Msalaba |
Lakini, malaika wa mama
Bikira Maria hakuwa Gisselle peke yake.
Kanisani hatukuelewa sana zaidi ya ufafanuzi wa vipeperushi ambavyo Gisselle
alinitafsiria. Tulipotoka kanisani, tulikutana na mama mmoja akiwa ameshika
bendera. Tulimsalimu mama yule na
kumuomba kumsaidia kushika bendera. Kisha Gisselle akamuuliza unasubiri
nini? akajibu wahujaji wapo kwenye
kikundi mimi ni muongozaji wao. Basi nasi tukakaa nae hapo akatuelezea historia
nzima kisha akasema tukae pale tuwasubiri wahujaji ili tuweze kwenda nao.
Tuliona bahati iliyoje kwani mstari wa kuingia pangoni ulikuwa ni mrefu sana.
Basi walipokuja wahujaji wengine tukaongozana, ajabu ni kwamba sisi hatukupanga
foleni, tulifunguliwa geti tukaingia pangoni. Lakini wakati naondoka Uswiss, nilikuwa nina maombi
mengi sana na niliyaandika kwenye karatasi. Karatasi kubwa ilijaa huku na huku
na bado nikadhani haitoshi lakini niliposogea eneo la hijani nikamwambia mama
" Mama mpenzi, nina maombi mengi sana hata wewe unayaona, yote haya ni ya
muhimu lakini ombi langu ni moja tu mama, "NIGUSE MOYO WANGU" Sasa
hata niliposogea karibu na Pango, nilimwambia mama kwamba "NIGUSE MOYO WANGU".
Pangoni |
Tulipoingia pangoni
nilipatwa na hali ambayo siwezi kuielezea, nilimfwata polisi na kuomba kupiga
picha lakini mikono yangu haikuweza ilitetemeka tu, sikusikia wala kuona watu
wengine nilijihisi nipo mimi tu, kiukweli siwezi kuelezea hali iliyonipata. Uso
wangu ulijaa machozi na sikuweza kufanya chochote. Tulipotoka Pangoni, yule
kiongozi akamwambia rafiki yangu kwa kifaransa Votre ami a reçu la bénédiction"
kwamba "Rafiki yako amepokea neema/ benediction". Maneno yale
sikuyaelewa mwanzoni lakini baada ya safari yote na kutafakari nilitambua
kwamba mama Maria alinipa zawadi niliyomuomba ya kunigusa moyo wangu.
Kesho yake tulibahatika
kuoga katika mabafu yale na niliombwa kuanzisha rozari wakati tunasubiria
foleni. Nilifanikiwa kupata Sakramenti ya kitubio na kusali misa kisha usiku wa
Jumapili tulipanda Treni kurudi Geneva tulipokuwa tukiishi na kuwasili Jumatatu
asubuhi. Kwakweli nina mengi ya kueleza lakini haya machache naamini ni zawadi
tosha.
Kijito alichovuka Bernadetha kwenda kumuona mama Bikira Maria Pangoni. Njia ya Pangoni na Visima vya kuoga |
Pd. Matanda na marafiki
wote, simulizi hii ni zawadi yangu kwenu. Mbarikiwe sana
Kwa upendo wa Kristu,
Vincenzia- Marie
No comments:
Post a Comment